Ndugu Waandishi,
Nalazimika kukutana nanyi kutoa maelezo juu ya tuhuma zenye shinikizo la kisiasa zinazoelekezwa kwangu binafsi kwamba hata mimi
nimeshiriki katika vitendo vya rushwa, kwa nafasi yangu kama Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma. Taarifa hizo, kama kawaida ya
uzushi mwingine wowote zimesambazwa kimkakati na kwa kasi kubwa kiasi
cha kuukanganya umma.
Nafahamu
nabeba dhamana kubwa ya uongozi, taswira yangu ya uongozi daima
imeakisi njozi na matumaini ya wananchi wa Kigoma Kaskazini, wananchi
wanyonge na vijana kote nchini bila kujali itikadi zao za kisiasa,
jinsia zao, makabila yao na rika zao. Hivyo, nawajibika kupitia kwenu
kuwatoa hofu juu ya hisia potofu zinazopandikizwa kwao na wale
wasiopenda kuona baadhi yetu tukiwaunganisha na kuwasemea watanzania
wasio na sauti, dhidi ya vitendo vya hujuma na vyenye dhamira ovu kwa
taifa.
Mkakati huo wa kuniunganisha na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaotuhumiwa kwa kupokea Rushwa unatekelezwa kwa njia zifuatazo:
-
Kumekuwa na kauli za watendaji wa serikali ambao wamekuwa wakizieneza
na hususan kutoa taswira kwamba baadhi ya kauli zangu zinatokana na
ushawishi wa rushwa;
-
Kuna taarifa ambazo zimeandikwa tena katika kurasa za mbele za baadhi
ya vyombo vya habari zikidai ’’Zitto kitanzini’’ ama ’’Zitto sawa na
popo nundu’’ zikiashiria kwamba na mimi ni mla rushwa; na
-
Waandishi wa habari na jamii kwa ujumla wamefikia kuaminishwa habari
hizi kiasi cha wengine kuuliza kwa nini Mhe. Zitto Kabwe hakutajwa
katika orodha iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani.
Ndugu Waandishi,
Naomba
kutoa ufafanuzi wa hicho kinachoelezwa kwamba nina ushiriki katika
masuala ya rushwa hususan kwenye masuala yanayohusu sekta ya Nishati na
Madini:-
- Mara
baada ya bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Usambazaji wa Umeme
Tanzania (TANESCO) chini ya Uenyekiti wake Meja Jenerali Mstaafu Robert
Mboma kutangaza kwamba imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika
hilo, Nd. William Mhando ili kupisha uchunguzi wa baadhi ya
vitendo/mwenendo wake, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC)
ambayo mimi ni Mwenyekiti wake ilimuandikia Mhe. Spika kumuomba aridhie
ili Kamati iweze kuwaita Bodi ya TANESCO, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Mahesabu ya Serikali (CAG) na pia Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya
Umma (PPRA) kujiridhisha na tuhuma zote zinazotajwa zinafanyiwa
uchunguzi wa kina na hatua kuchukuliwa;
- Kamati
ya POAC ninayoiongoza ilimuomba Mhe. Spika kuwaita wahusika tajwa kwa
kuwa zilikuwapo tetesi kuwa kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi huyo siku
chache kabla ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kulikuwa na lengo
la kufunika ’madudu’ makubwa zaidi kwa kulichagiza Bunge na tukio hilo
dogo, mkakati ambao naona umefanikiwa sana.
Isitoshe, Kamati kutaka kujiridhisha na hatua za Bodi ni sehemu ya
msingi ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati yaliyowekwa kwa mujibu wa
Kanuni za Kudumu za Bunge na pia Shirika la TANESCO ni moja kati ya
mashirika ambayo yanawajibika kwetu kwa hesabu zake na pia ufanisi wake
kwa ujumla. Tumefanya hivyo pia katika mashirika mengine, hili la
TANESCO sio tukio la kipekee;
- Kitendo
hiki cha halali na kwa mujibu wa Kanuni kilichofanywa na Kamati yangu
kimetafsiriwa kwa makusudi na baadhi ya watu kwamba ni ishara ya kuwa
sisi au zaidi kwamba mimi nina maslahi binafsi na TANESCO na hususan
Mkurugenzi wake Injinia Mhando, ndio maana tumetaka maelezo ya Bodi.
Ukweli kwamba Kamati ya POAC tumewaita pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Mahesabu (CAG) na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa
jambo hilo hilo umefichwa kwa makusudi!
- Baada
ya tukio hilo, nikiwa hapa Dodoma, mwandishi wa habari wa gazeti moja
alinifuata akiniambia kuwa wamekutana na Mhe. Waziri Mhongo na Katibu
Mkuu wake, Nd. Eliachim Maswi hapa hapa Bungeni na wamewaambia kuwa mimi
nimepewa rushwa. Hakutaja nimepewa rushwa na nani, kiasi gani na wala
kwa lengo gani!
- Nimejaribu
kumtafuta kwa simu Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu wake ili wanipe
ufafanuzi juu ya mimi na Kamati ya POAC kuhusishwa na tuhuma hizi bila
mafanikio, hali ambayo inaniondolea mashaka juu ya ushiriki wao katika
kueneza au kuthibitisha uvumi huo. Najaribu sana kujizuia kutokuwa na
mashaka na ushiriki wao huo ikizingatiwa uzito na taswira ya nafasi zao
katika jamii, lakini wameshindwa kunidhihirishia tofauti.
Sasa
naomba kutoa ufafanuzi rasmi kuhusu mlolongo wa matukio hayo tajwa
ambayo yanatumiwa na baadhi ya wanasiasa kuonesha kwamba eti nimehusika
na vitendo vya rushwa.
- Binafsi
sijawahi kuwa na mawasiliano ya aina yeyote na uongozi wa TANESCO
kushawishiwa juu ya hatua ambazo POAC ndio imezichukua za kutaka
kujiridhisha juu ya utaratibu uliotumika. Ieleweke wazi kabisa kuwa,
hakuna wakati wowote, popote ambapo mimi binafsi au Kamati yetu imekataa
Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO kuchunguzwa kwa tuhuma zozote. Ambacho
tumesisitiza wakati wote ni ufuatwaji wa taratibu, kanuni na sheria,
hili nitalisimamia iwe masika au kiangazi;
- Ni
kwa sababu hiyo, na kwa kujiamini kabisa nimeunga mkono suala la tuhuma
za rushwa zinazotajwa zichunguzwe na Kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge kwa kina;
- Nimekwenda
mbali zaidi kukiomba chama changu CHADEMA kifanye pia uchunguzi na
tathmini yake kwa kina kujiridhisha na tuhuma hizo;
- Natumia fursa hii pia kuomba vyombo vya Dola vichunguze tuhuma hizo kwa nafasi yake ili kuweza kupata ukweli;
- Ninaahidi
kushiriki kikamilifu iwapo nitatakiwa katika uchunguzi wowote
utakaofanywa na niko tayari kuwajibika iwapo nitakutwa na hatia yeyote.
Napenda
niwatoe hofu wananchi wa jimbo la Kigoma Kaskazini walionituma kuja
kuwawakilisha hapa Bungeni na Watanzania wote kwa ujumla kwamba:-
- Mimi
Zitto Zuberi Kabwe sina bei, sijawahi kuwa nayo na sitarajii kuwa nayo
huko mbeleni. Daima nimesimamia kidete maadili ya uongozi bora katika
maisha yangu yote ya siasa, na nawaahidi sitarudi nyuma katika mapambano
dhidi ya rushwa katika nchi hii pamoja na mikakati ya aina hii ya
kunidhoofisha na kunivunja moyo;
- Nafarijika
na salam mbali mbali zinazotolewa kunifariji na kusisitiza kuwa
nisilegeze kamba katika mapambano haya, nimepokea ujumbe mwingi kwa
simu, sms, tweeter na hata facebook na niko pamoja nanyi Watanzania
wenzangu kamwe sitarudi nyuma hadi kieleweke. Naamini
katika nchi yetu tunazo rasilimali za kutosha mahitaji/haja ya kila
mmoja wetu lakini si ‘tamaa/ulafi’ wa baadhi ya watanzania wenzetu;
- Napenda
kuweka rekodi sawa kwa Watanzania kwamba nimekuwa Mbunge hiki ni
kipindi cha pili, Mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya
Umma (POAC) huu ni takriban mwaka wa saba sasa, Kamati yangu inasimamia
mashirika 259 ya Umma na si TANESCO peke yake. Mchango wa Kamati hii
katika Bunge na kwa ustawi wa Mashirika ya Umma ni bayana na haujawahi
kutiliwa shaka. Kamati yetu imeokoa upotevu mkubwa wa mali za umma na
kuokoa fedha za umma kutokana na umakini wake. Tumefanya hivyo CHC hivi
karibuni, Kiwira na kwenye mashirika mengine mengi. Kote huko uadilifu
na uzalendo wa Kamati hii haujawahi kuhojiwa. Inatuwia vigumu kuona kuwa
tunahojiwa katika suala hili la TANESCO. Hapa pana kitendawili.
- Zipo
hoja pandikizi za kutaka Kamati ya POAC ivunjwe na haswa zikinilenga
mimi binafsi. Nafahamu kiu ya wasioitakia mema nchi yetu kuiona POAC
ikivunjwa au sura zikibadilishwa kwa kuwa Kamati hii imekuwa mwiba kwa
mikakati yao ya kifisadi. Kwa maoni yangu, Kamati ya POAC isihusishwe na
tuhuma hizi kwa vyovyote vile. Niko tayari nihukumiwe mimi kama mimi na
sio kuhusisha wajumbe wengine ambao hawatajwi mahala popote katika
tuhuma hizi mbaya sana katika historia ya Bunge letu. Nitakuwa tayari
kunusuru Kamati ya POAC na maslahi ya taifa letu kwa kujiuzulu Uenyekiti
iwapo itathibitika pasipo shaka kuwa nimehongwa. Kamati ya POAC ni
muhimu zaidi kuliko mimi.
- Nafahamu
pia kuwa kuna wanasiasa hasa wa Upinzani ambao wanautaka sana Uenyekiti
wa POAC na wanafanya kila njia kutaka kuidhoofisha. Lakini hawajui kuwa
anaepanga wajumbe wa Kamati ni Spika wa Bunge.
- Msishangae
pia kuja baadae kubaini kwamba baadhi ya wanasiasa wenye midomo mikubwa
ya kutuhumu wenzao wao ndio vinara wa kupokea rushwa.
- Ni
lazima tufike mahali kama viongozi kwamba utaratibu unapokiukwa na
yeyote yule, au uongo unapotolewa hadharani tuseme bila kuogopa. Hili
ndio jukumu letu kama wabunge na viongozi. Kusimamia ufuatiliaji wa
utaratibu ni jukumu letu kama Kamati ya POAC na ndio sababu ya msingi ya
kuanzishwa kwa mamlaka kama CAG na PPRA. Haiwezekani, tuwe na set ya
kanuni kwa kundi fulani na nyingine kwa makundi mengine, au kuhukumu
ufuataji wa taratibu kwa kuangalia sura ya mtu usoni
Mwisho
Kumejengeka
tabia hivi sasa ya kuwamaliza wanasiasa wenye kudai uwajibikaji na
uzalendo. Kumeanzishwa kiwanda kwenye medani ya siasa cha kuzalisha
majungu na fitna zenye lengo la kuwachonganisha wanasiasa wa aina hiyo
na wananchi kwa kutumia vyombo vya habari na nguvu ya fedha. Naamini
mbinu hizi chafu, kama nyingine nyingi zilizojaribiwa kwangu huko nyuma
nazo zitashindwa.
Naamini
katika kweli na kweli daima huniweka huru. Naamini kuwa mwale mdogo wa
mwanga wa mshumaa hufukuza kiza. Kwa imani hiyo, sitasalimu amri mbele
ya dhamira zao ovu hata nitakapobaki peke yangu katika mapambano hayo ya
kulinda na kutetea rasilimali za taifa zinufaishe watanzania wote.
Daima
nitaongozwa na busara ya Hayati Shabaan Robert isemayo, ‘Msema kweli
huchukiwa na marafiki zake, nitakapofikwa na ajali hiyo, sitaona wivu
juu ya wale wawezao kudumu na marafiki zao siku zote, siwezi kuikana
kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo, nikajitenga na furaha ya kweli
itakayotokea pale uwongo utakapojitenga”.
Ahsanteni sana
0 comments:
Post a Comment